Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Msichana mwingine abakwa na kuuawa India, UNICEF yatoa tamko

Msichana mwingine abakwa na kuuawa India, UNICEF yatoa tamko

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF limerejelea wito wa kutaka haki itendeke huko India kwenye jimbo la Uttar Predesh baada ya ripoti za kubakwa na kuuawa hii leo kwa mtoto mwingine wa kike mwenye umri wa miaka 13.

Ripoti hizo zinakuja wiki moja baada ya tukio lingine la watoto wawili wa kike kubakwa na kundi la watu na hatimaye kuuawa kwenye jimbo hilo hilo ambapo UNICEF imesema haikubaliki.

Taarifa ya shirika hilo imetaka haki itendeke kwa waathirika wa uhalifu huo na familia zao pamoja na watoto wa kike duniani kote ambao wanatumbukia kwenye ukatili wa kingono.

UNICEF imesema hakuna jambo lolote linaloweza kuhalalisha kitendo hicho au hata kuwezesha watekelezaji kukwepa mkono wa sheria kwani kitendo hicho sio tu kinaathiri wasichana na wanawake bali kinaweka mpasuko kwenye jamii.

Imesema hakuna kinachoweza kurejesha uhai wa wasichana waliokufa huko Uttar Pradesh lakini kinachoweza kufanyika ni kila mmoja kuazimia kuhakikisha haki ya mtoto ya kuishi maisha salama na yenye utu inazingatiwa na kwamba ukatili dhidi ya mtoto ni kosa.