Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Visa vipya vya Ebola vyaripotiwa Afrika Magharibi,lakini hakuna zuio la safari au biashara:WHO

Visa vipya vya Ebola vyaripotiwa Afrika Magharibi,lakini hakuna zuio la safari au biashara:WHO

Shirika la afya duniani, WHO limesema watu 21 wanasadikiwa kufariki dunia kutokana na Ebola huko Guuinea na Liberia kati ya tarehe 29 Mei na Juni Mosi mwaka huu ambapo idadi hiyo ni kati ya visa 51 vilivyoripotiwa nchini humo na Sierra Leone.

WHO inasema Guinea inaongoza kwa kuwa na wagonjwa wengi kwenye kwenye mji mkuu Conakry ambako hadi sasa watu waliothibitishwa kufariki dunia kutokana na ugonjwa huo imefikia 80 kati ya vifo 328.

Nchini Sierra Leone nako licha ya kwamba hakuna vifo vipya kati ya muda huo lakini kumekuwepo na visa vipya 13 ambapo wagonjwa watatu wamethibitishwa kufariki dunia kwa Ebola.

Hata hivyo WHO inasema idadi kamili ya vifo kutokana na Ebola inaweza kubadilika kutokana na uchunguzi wa maabara unaoendelea dhidi ya washukiwa wa ugonjwa huo wakati huu ambapo usimamizi pia na huduma za utabibu zimeimarishwa.

Mathalani nchini Guinea wataalamu wa ziada watano wamepelekwa kwenye maeneo ya Gueckedou and Macenta ili kusaidia kituo cha afya ya jamii kwenye uchambuzi wa takwimu. Huko Sierra Leone wahudumu wa afya kwenye maeneo ya mlipuko wanapatiwa amfunzo ya utoaji huduma kwa wagonjwa wa Ebola ili kudhibiti maambukizi mapya.

WHO imesisitiza kuwa kwa misingi ya taarifa za ugonjwa wa Ebola kwa sasa, bado haijatoa pendekezo lolote la zuio la safari au biashara na nchi hizo za Guinea, Liberia, na Sierra Leone.