Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baada ya kukimbia hatari CAR, watoto na wanawake hawapaswi kukumbwa na machungu ya njaa:UM

Wakati wa kupatia watoto wa wakimbizi lishe bora kwenye kituo kimoja cha afya huko Cameroon.(@UNHCR / F.Noy )

Baada ya kukimbia hatari CAR, watoto na wanawake hawapaswi kukumbwa na machungu ya njaa:UM

Mashirika ya Umoja wa Mataifa yanayohusika na usaidizi wa kibinadamu yamesema wananchi wanaokimbia mapigano huko Jamhuri ya Afrika ya Kati na kusaka hifadhi Cameroon hawapaswi kukumbwa tena na machungu mengine. Taarifa kamili na John Ronoh.

(Taarifa ya John)

Wakizungumza mjini Roma Italia, Kamishna mkuu wa UNHCR linalohusika na wakimbizi Antonio Guterres na Mkurugenzi Mkuu wa WFP linalohusika na mpango wa chakula duniani, Ertharin Cousin wamesema wengi wa wakimbizi hao wanawasili wakiwa wamechoka na wagonjwa.

Mathalani Cousin amesema wakimbizi hao hususan wanawake na watoto wanakabiliwa na ukosefu wa chakula na hivyo kuwaweka hatarini kupata utapiamlo jambo ambalo wamesema hawastahili.

Halikadhalika Guterres amesema kwa kuwa tayari wamekimbia shida, ni lazima mahitaji yao ya dharura ikiwemo chakula yatimizwe ili kuepusha uwezekano wa kufa kwa njaa.

Takwimu zinaonyesha kuwa kila wiki watu Elfu Mbili huwasili Cameroon wakitokea Jamhuri ya Afrika ya Kati na wengi wao ni wanawake na watoto, ambapo kiwango cha utapiamlo wa kupindukia ni kati ya asilimia 20 na 30.

Tayari WFP imeanza operesheni ya dharura ya kulisha watu Laki Moja nchini Cameroon na inatafuta dola Milioni 15 ili kufanya kazi hiyo ndani ya miezi minane.

Kwa sasa mpango wa kikanda wa kusaidia wakimbizi Jamhuri ya Afrika ya Kati umepatiwa asilimia Tisa tu ya fedha zinazohitajika. Nchi Wakimbizi hao ni wale waliosaka hifadhi Cameroon, Chad, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na

Congo-Brazaville.