Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zaidi ya wahamiaji 40,000 wameingia Italia kwa njia ya meli mwaka huu

(Ramani@IOM)

Zaidi ya wahamiaji 40,000 wameingia Italia kwa njia ya meli mwaka huu

Idadi ya wahamiaji wanaovuka bahari ya Mediterania kuingia Italia imeongezeka mwaka huu ambapo Shirika la Kimataifa la Uhamiaji, IOM linasema mwaka huu pekee imefikia 40,000 sawa na idadi ya walioingia nchini humo mwaka mzima wa 2013. Christiane Berthiaume, msemaji wa IOM, anaeleza sababu za ongezeko hilo.

“ Serikali ya Italia imeanzisha mfumo huo wa MareNostrum, ni operesheni kubwa, ikiwa na meli kubwa sana zinazozingira bahari ya Mediterania siku zote, usiku na mchana, kwa ajili ya kuokoa wahamiaji wanaosafiri kwenye meli zisizo imara na kuwapeleka kwenye kisiwa cha Sicilia. Lakini pia watu wengi hao wametoka Libya na hawataki tena kubaki nchini humo kwani hali ya usalama huko ni mbaya”

Amesema, IOM inaunga mkono mpango huo wa Italia huku akisema kuwa idadi ya wahamiaji wanaoingia nchini humo si ya kushtusha sana, ikilinganishwa na idadi ya wahamiaji 120 000 wanaopokelewa Ujerumani na wale 65 000 wanaoingia Ufaransa kila mwaka.

Christiane amesema wahamiaji wengi wametoka Niger, Somalia, Morocco, Ethiopia, Syria na lengo lao ni kutafuta maisha mazuri zaidi.

“ Mtu ambaye ameamua kupanda meli hizo, na kuweka maisha yake hatarini na yale ya watoto wake na mke wake, huyu mtu amekata tamaa na maisha. Kwa hiyo IOM inaomba nchi zinazopokea wahamiaji wakae pamoja na nchi wanakotoka wahamiaji hawa kujadili na kutafuta suluhu ya kudumu kwa tatizo la uhamiaji”