Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

ICC yamhukumu kiongozi wa waasi DRC kifungo cha miaka 12 jela

German Katanga wakati wa hukumu yake hii leo huko The Hague, Uholanzi. (Picha: © ICC-CPI)

ICC yamhukumu kiongozi wa waasi DRC kifungo cha miaka 12 jela

Mahakama ya kimataifa ya uhalifu, ICC huko The Hague, Uholanzi leo imemhukumu kifungo cha miaka 12 jela Germain Katanga aliyepatikana na hatia ya makosa ya  uhalifu dhidi ya binadamu na uhalifu wa kivita huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.

Akisoma hukumu hiyo Jaji Bruno Cotte amesema wamezingatia mahitaji ya kisheria, ukweli na haki kwa wahanga wa uhalifu uliotekelezwa na familia zao na kuhakikisha kuwa hukumu hiyo itaepusha wanaotaka kutekeleza vitendo hivyo wasifanye hivyo.

Hata hivyo mahakama imeeleza kuwa muda ambao Katanga alikuwepo rumande kuanzia Septemba 2007 hadi Mei 2014 utapunguzwa katika adhabu hiyo ya kifungo cha miaka 12. Halikadhalika imesema kulingana na mazingira hakutakuwepo na faini yoyote dhidi ya Katanga.

Mwezi Machi mwaka huu Katanga alipatikana na hatia ya makosa matano ikiwemo moja ya uhalifu dhidi ya binadamu na Manne ya uhalifu wa kivita ikiwemo kushambulia raia na uharibifu wa mali.

Ilithibitishwa pasipo shaka kuwa Katanga alichangia kwa kiasi kikubwa kwa vitendo vilivyotekelezwa na wanamgambo wa Ngiti huko Bogoro jimbo la Ituri Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, mwezi Februari mwaka 2003.

Kesi dhidi ya Katanga ilianza tarehe 24 Novemba 2007.