Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ufadhili wa kibinadamu uongezwe Somalia: Nicholas Kay

Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu na Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa nchini Somalia, UNSOM, Nicholas Kay

Ufadhili wa kibinadamu uongezwe Somalia: Nicholas Kay

Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu na Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa nchini Somalia, UNSOM, Nicholas Kay, amesema kuna haja ya kutoa ufadhili wa dharura ili kusaidia kukabiliana na hali mbaya ya kibinadamu nchini humo, akiongeza kuwa bila ufadhili zaidi Wasomali wengi wamo hatarini kutumbukia mashakani hata zaidi.

Bwana Kay amesema hofu yake ni kwamba, wanawake, watoto na watu wengine wanyonge wataanza kupata matatizo yatokanayo na ukosefu wa huduma za afya na chakula, akitaja hali hiyo kuwa ni ya dharura.

Kwa mujibu wa Ofisi ya kuratibu Masuala ya Kibinadamu, mahitaji ya kibinadamu nchini Somalia yamepata asilimia 15 tu ya ufadhili unaohitajika, huku kukiwa na kasoro ya dola milioni 790 kwa fedha zinazohitajika mwaka huu.

Bwana Kay amesema anasikitika kwamba kuna uwezekano wa kuwepo uhaba wa chakula katika miezi michache ijayo, kwa sababu ya hali ya hewa na hali itokanayo na mashambulizi ya Al Shabaab yanayokatiza uchukuzi wa chakula mijini.