Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF yapatiwa Euro Milioni 4.5 kuimarisha usaidizi kwa watoto Sudan Kusini

Watoto wakimbizi wa Sudan Kusini © UNICEF Sudan Kusini/2014/Pires

UNICEF yapatiwa Euro Milioni 4.5 kuimarisha usaidizi kwa watoto Sudan Kusini

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limepatiwa Euro Milioni 4.5 na tume ya Muungano wa Ulaya ya masuala ya dhaura na usamaria mwema (ECHO) ili kuimarisha msaada wake wa dharura Sudan Kusini.

Taarifa zinasema kati ya wakimbizi Milioni Moja nchini humo, nusu yao ni watoto ambao wanahitaji misaada ya dharura.

Mwakilishi wa UNICEF Sudan Kusini, Jonathan Veitch, alishikuru kwa ufadhili wa ECHO akisema zaidi ya watoto 50,000 wako hatarini ya kufa kwa njaa mwaka huu, misaada ikichelewa kuwafikia.

Msaada huu utachangia katika miradi ya UNICEF ya kuwapatia wakimbizi hao maji, vyoo, chanjo za surua, na chakula maalum kwa watoto walioathirika na utapiamlo, pamoja na sehemu maalum kwa watoto walioteseka na mzozo.

Kwa mujibu wa ECHO, muungano wa Ulaya umeshatoa zaidi ya euro milioni 130 kwa misaada ya kibinadamu.