Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkutano wa nchi zinazoendelea zisizo na bahari kufanyika Novemba Austria

Mkutano wa nchi zinazoendelea zisizo na bahari kufanyika Novemba Austria

Msaidizi wa Katibu Mkuu anayehusika na masuala ya nchi zinazoendelea ambazo hazipakani na bahari, Gyan Chandra Acharya, amesema kuwa mkutano wa Umoja wa Mataifa utakaofanyika mwezi Novemba kuhusu nchi hizo nchini Austria, utalenga kuzisaidia nchi hizo kukabiliana na changamoto za biashara na usafiri ambazo zinakumbana nazo.

“Tatizo lao kubwa ni kwamba, kwa sababu hazipo karibu na ufuko wa bahari, uchukuzi wa bidhaa ni mgumu, na biashara yao pia inatatizika, na maendeleo ya miundo mbinu pia ni changamoto kubwa kwao. Nchi hizi zinalipa takriban mara mbili ya gharama ya kufanya biashara, idadi ya siku zinazochukua kusafirisha shehena ya mizigo kutoka nje, ni karibu mara mbili ya muda wa kawaida unaochukuliwa katika usafiri huo katika nchini nyingine, na hili linaathiri ukuaji wa kiuchumi.”

Bwana Acharya amesema Umoja wa Mataifa umekuwa ukisaidia katika kuona kuwa malengo ya maendeleo ya nchi wanachama wa kundi hilo ambazo ni 32 kwa jumla yanatimizwa, na kwamba kongamano la Novemba litafanya tahmini ya maendeleo yaliyofanywa tangu mwaka 2003, kuhusu jinsi hali ya ushirikiano na nchi zinakopitisha mizigo yao umekuwa, jinsi zimeongeza wigo wa biashara zao, jinsi miundo mbinu yao imeendelezwa kutokana na ubia ambao umekuwepo, na usaidizi wa kimataifa unaoweza kutolewa kwao.

Ameongeza kuwa masuala ya athari za mabadiliko ya tabianchi na mdororo wa kiuchumi, ambayo hayakuwepo mwaka 2003, pia yataangaziwa, pamoja na ushirikiano wa kikanda.