Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

Shirika la UM juu ya Ilimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) jana lilimaliza Mkutano wa Dunia juu ya Iimu ya Juu uliofanyika Paris, ambapo kulitolewa mwito maalumu unaozitaka nchi wanachama kuongeza mchango wao katika juhudi za kukuza ilimu. Kwenye taarifa rasmi ya mkutano, wajumbe waliowakilisha nchi 150 walitilia mkazo umuhimu wa kuwekeza posho ya bajeti lao kwenye sekta ya ilimu, ili kujenga jamii yenye maarifa anuwai, na inayomhusisha kila raia, ambaye atapatiwa fursa sawa ya kushiriki kwenye tafiti za hali ya juu, huduma itakayowakilisha uvumbuzi na ubunifu wenye natija kwa umma.

Ijumamosi, tarehe 11 Julai ni Siku ya Udhibiti wa Idadi ya Watu Duniani. Shirika la UM juu ya Udhibiti wa Idadi ya Watu (UNFPA) ilieleza kwenye taarifa kwa waandishi habari juu ya siku hiyo kwamba uwekezaji wenye kulenga maendeleo ya wanawake ndio mradi wenye fursa ya kuandaa mazingira imara, yatakayosaidia kufufua uchumi, kupunguza umasikini na kukomesha utovu wa usawa wa kijinsia. Kwa mujibu wa UNFPA afya za wanawake zinajumuisha mchango muhimu wa kiuchumi katika nchi zinazoendelea, ambapo imeoenekana wanawake hujumlisha nusu ya wafanyakazi katika sekta ya kilimo. Kwa mfano, katika bara la Afrika wanawake ndio wenye kuhusika na asilimia 80 ya shughuli za kupandisha mazao makuu, na katika nchi za Asia za Kusini-Mashariki asilimia 90 ya wakulima wa mpunga ni wanawake.