Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vitabu vinaweza kutokomeza umaskini na kujenga amani: UNESCO

Vitabu vinaweza kutokomeza umaskini na kujenga amani: UNESCO

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO, Irina Bokova, amesema kuwa vitabu vina uwezo mkubwa wa kutokomeza umaskini na kujenga amani. Bi Bokova amesema hayo kabla ya Siku ya Vitabu na Hati Miliki Duniani, ambayo itasherehekewa mnamo Aprili 23, kwa maonyesho kwenye makao makuu ya UNESCO, kuadhimisha miaka 50 ya kibogoyo aitwaye Mafalda, ambaye aliundwa na msanii Quino, raia wa Argentina. Maonyesho mengine yatakuwa ya manga, maandishi ya kiarabu na kiajemi, pamoja na yale ya nchi za Magharibi.

Mnamo siku hiyo, UNESCO pia itazindua ripoti kuhusu kusoma katika enzi za vidude vya viganjani. Ripoti hiyo ni ya uchunguzi kuhusu uwezekano wa vidude vya mawasiliano vya kiganjani kuwa vyombo vya kusoma katika maeneo mengi duniani ambako watu wengi hawawezi kumudu kununua vitabu.

Kutakuwa pia na mashindano ya watoto wenye umri wa kati ya miaka 6 na 13, yaitwayo, ‘Tengeneza jalidi lako mwenyewe.’

Siku hiyo pia, mji wa Port Harcourt nchini Nigeria utatangazwa kuwa Mji Mkuu wa Vitabu Duniani kwa mwaka 2014. Lengo, amesema Bi Bokova, ni kuwapa msukumo waandishi na wasanii kuhakikisha kuwa wanawake na wanaume wengi zaidi wananufaika kutokana na kujua kusoma na kuandika katika njia zinazoweza kupatikana kwa urahisi.