Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Malengo mapya ya elimu duniani yatoe kipaumbele kwa wasichana: UNESCO

Malengo mapya ya elimu duniani yatoe kipaumbele kwa wasichana: UNESCO

Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO, limesema kuwa hali mbaya ya kutokuwa na usawa katika elimu duniani imewaacha zaidi ya watoto wa kike milioni 100 katika nchi za kipato cha chini na cha wastani bila uwezo wa kusoma hata angalau sentensi moja.

Hayo yameibuka katika ripoti ya utafiti ulofanywa na UNESCO kuhusu elimu kwa wote, ambayo imesema hali hiyo pia itawazuia nusu ya watoto wa kike milioni 31 ambao hawapo shuleni sasa hivi kupata fursa ya kuwahi kufanya hivyo.

Ripoti hiyo ambayo imezinduliwa kama sehemu ya maadhimisho ya

Siku ya Kimataifa ya Wanawake kwa ushirikiano na Mkakati wa Umoja wa Mataifa wa Elimu kwa Wasichana, UNGEI, inatoa wito usawa upewe kipaumbele katika malengo mapya ya maendeleo baada ya mwaka 2015, ili kila mtoto awe na fursa sawa ya kufundishwa kupitia elimu bora.

Ripoti inasema licha ya hatua zilizopigwa, kufikia mwaka 2011, ni asilimia 60 tu y anchi ndizo zilikuwa zimefikia usawa katika elimu ya msingi, huku asilimia 38 tu zikifikia usawa katika shule za sekondari.

Katika nchi za kipato cha chini, ni asilimia 20 tu ya usawa ilikuwa imefikiwa katika shule za msingi, na asilimia 8 tu katika shule za sekondari. Watoto wa kike katika nchi za Kiarabu ndio walioathiriwa mno, zikifuatiwa na kusini na magharibi mwa Asia, na kisha Afrika.