Baraza la Usalama laazimia kuimarisha ujumbe wa UNAMID

3 Aprili 2014

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataidfa, leo kwa kauli moja limepitisha azimio la kuimarisha ujumbe wa pamoja wa Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika kuhusu eneo la Darfur, UNAMID, na kufanyia marekebisho majukumu yake. Joshua Mmali na taarifa kamili

Taarifa ya Joshua

Azimio hilo namba 2148/2014. limetokana na mswada uliowasilishwa na Australia, Ufaransa, Luxembourg, Nigeria, Lithuania, Korea Kusini, Uingereza na Marekani, kufuatia ripoti ya Katibu Mkuu ya Februari 25 2014, ilotoa mapendekezo ya kufanyia marekebisho majukumu ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa Darfur, UNAMID, na kuuimarisha ujumbe huo.

Baraza hilo limeyakubali mapendekezo hayo yote, na kwa mujibu wa azimio la leo, merekebisho yatafanyiwa majukumu ya kipaumbele ya ujumbe wa UNAMID, yakiwemo ulinzi wa raia, kuwezesha utoaji wa misaada ya kibinadamu na usalama wa wahudumu wa kibinadamu, na katika kusaidia juhudi za upatanishi baina ya serikali ya Sudan na makundi yenye silaha.

Pamoja na hayo, UNAMID itahitajika kusaidia katika juhudi za upatanishi miongoni mwa jamii zinazozozana, na kukabiliana na vianzo vya migogoro baina yao. Mwakilishi wa Sudan kwenye Umoja wa Mataifa, amesema haya baada ya kupitishwa azimio hilo.

“Tumeitathmini ripoti ya Katibu Mkuu kuhusu UNAMID, na tunakubaliana na hatua ya kuimarisha ujumbe huo, tukizingatia hatua za ufanisi zilizopatikana sasa katika mzozo wa Darfur, ambazo zinahitaji kufanyia marekebisho utaratibu wa UNAMID na majukumu yake ili kusaidia kuendeleza juhudi za kuleta utulivu na kuchangia juhudi za kumaliza mapigano ya kikabila yaliyotokea hivi karibuni, na hivyo kuzorotesha hali ya usalama”