Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Pamoja na kukumbuka utumwa, tumulike utumwa wa sasa na kuutokomeza: Dtk. Ashe

Pamoja na kukumbuka utumwa, tumulike utumwa wa sasa na kuutokomeza: Dtk. Ashe

Tukio maalum la kukumbuka wahanga wa utumwa na wa biashara ya utumwa kupitia Atlantiki limefanyika kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa siku ya Jumanne siku ya kimataifa ya kukumbuka tukio hilo.

Kauli mbiu ya mwaka huu ni "Ushindi dhidi ya utumwa:Haiti na kwingineko.

Rais wa Baraza Kuu Dkt. John William Ashe akizungumza kwenye tukio hilo amesema utumwa ulikuwa ni kitendo dhalili ambacho kamwe hakipaswi kurejewa akitaja vile ambavyo wananchi wa Haiti walivyoendesha mapinduzi katiya mwaka 1791 na 1804, mapinduzi ambayo amesema yaliweka historia ya aina yake Amerika hadi Ulaya na hata kuzaliwa kwa taifa la Haiti.

Hata hivyo amesema wakati jamii ya kimataifa inakumbuka utumwa wa enzi hizo ni lazima kumulika ukatili unaendelea zama za sasa kwa njia mbali mbali . amesema wanawake na wasichana sehemu mbali mbali duniani wanawekwa rehani na kunyimwa uhuru wao wa msingi huku watoto wakigeuzwa watwana na kutumikishwa.

Amesema kukabiliana na hali hiyo ni changamoto kubwa lakini…

(Sauti ya Ashe)

“Kama jumuiya ya kimataifa ni wajibu wetu kushughulikia chanzo cha utumwa wa zama za sasa na kuwapatia usaidizi na ulinzi unaotakiwa wahanga wake. Halikadhalika tuhakikishe wahusika hawakwepi sheria. Kwa kuendeleza na kuimarisha juhudi zetu kutokomeza utumwa, wa sasa na ubaguzi wa aina zote ikiwemo wa rangi, tunakuwa tunachukua njia ya utu na heshima ya haki za binadamu na uhuru kwa watu wote.”