Baraza la Haki za binadamu lamulika ukatili wa kingono DRC.

25 Machi 2014

Baraza la haki za binadamu leo limepokea ripoti kuhusu ukatili wa kingono huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC ambapo limetaka hatua zichukuliwe kusaidia wahanga. Taarifa zaidi na Priscilla Lecomte.

(Taarifa ya Priscilla)

Akihutubia kikao hicho, Kamishna Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa, Navi Pillay, amesema ukatili wa kingono bado unafikia hatua ya kushtusha, hasa kwenye jimbo la Mashariki, lakini pia katika nchi nzima. Amesisitiza kwamba watekelezaji wa vitendo hivo wanakwepa sheria, na wahanga wananyanyapaliwa katika jamii.

(Sauti ya Pillay)

"Ofisi yangu imekuwa ina hofu kubwa juu ya ukosefu wa mfumo wa fidia kwa wahanga wa ukatili wa kingono. Ripoti ya jopo inasisitiza kuwa mara nyingi wahanga waliachwa wakiendelea kuathirika na machungu ya madhila ya ukatili huo. Jopo limependekeza hatua kadhaa ikiwemo kuanzishwa kwa mfuko wa fidia kukidhi mahitaji ya wahanga hao.”

Wivine Mumba Matipa ni Waziri wa Sheria na Haki za Binadamu wa DRC amesema kwamba nchi yao bado iko kwenye hali ya kujijenga baada ya vita. Changamoto ni nyingi ili kuwezesha wanawake,ambao ni asilimia 98 ya waathirika na ukatili wa kingono waweze kupewa haki zao.

(Sauti ya Matipa)

Kwa mujibu wa WAziri huyo serikali ya DRC imezindua mkakati wa kupinga ukatili wa kijinsia na sasa mahakama zote hadi ngazi za mitaa na mashirika madogo yasiyo ya kiserikali yanapatiwa mafunzo kuhusu jinsi ya kukabiliana na ukatili wa kingono.