Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Teknolojia mpya yasaidia kuharakisha uchunguzi dhidi ya TB:WHO

Teknolojia mpya yasaidia kuharakisha uchunguzi dhidi ya TB:WHO

Leo ni siku ya Kifua Kikuu duniani ambapo Shirika la Afya ulimwenguni, WHO linasema ujumbe mkuu ni kufikia watu Milioni Tatu walio kwenye mazingira magumu ya kuchunguza vyema afya zao kama njia muhimu ya kudhibiti ugonjwa huo.

Idadi hiyo kwa mujibu wa WHO ni theluthi Moja ya watu wote wanaoambukizwa Kifua Kikuu duniani kila mwaka.

WHO inasema uchunguzi wa mapema na tiba ya haraka ni muhimu kwani inaongeza fursa ya mgonjwa kupata tiba sahihi na kupona na hivyo kusaidia kudhibiti kusambaa kwa Kifua Kikuu sugu.

Kwa sasa shirika hilo linajivunia mradi mpya wa kubaini TB mapema uitwao EXPAND-TB unaotekelezwa katika nchi 27 zikiwemo Uganda, Msumbiji na Tanzania.

Mradi huo unatumia teknolojia mpya ya uchunguzi ambapo muda wa mgonjwa kupata majibu ya uchunguzi umepunguzwa hadi saa Mbili na Nusu ilhali kwa teknolojia ya zamani kuna maeneo ambako mpaka mgonjwa apate majibu ya uchunguzi huchukua hadi Miezi Miwili na Nusu.

Dokta Mario Raviglione ni Mkurugenzi wa mradi wa kimataifa wa kukabiliana na TB kwenye WHO na anasema licha ya mradi huo mpya bado kuna mambo ya kuzingatia.

(Sauti ya Dkt. Raviglione)

“Kuna ngazi kadhaa za kuzingatia wakati huu ambazo ni muhimu ili kuboresha mbinu za kubaini ugonjwa na siyo tu kubaini bali pia tiba sahihi, kwa sababu kile kinachoendelea kwenye sekta binafsi hakuna anayefahamu. Na tuna shuku kutokana na tafiti mbali mbali kuwa mara nyingi tiba dhidi ya TB hazikidhi viwango vya kimataifa vya matibabu, ni jambo ambalo siyo zuri ambalo siyo tu kwamba halitamtibu mgonjwa bali linachochea usugu kwa dawa.”

Halikadhalika Dokta Raviglione amesema gharama ya kutibu TB sugu ni kubwa kuliko TB ya kawaida, kwa hivyo ni vyema watu kujitokeza kuchunguzwa afya zao ili kupunguza mzigo wa gharama siyo tu kwa taifa husika bali hata kwa familia ya mgonjwa.