Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maendeleo ya wanawake na wasichana bado yana mkwamo licha ya mafanikio:CSW58

Maendeleo ya wanawake na wasichana bado yana mkwamo licha ya mafanikio:CSW58

Mkutano wa 58 wa Kamisheni ya juu ya hadhi ya wanawake duniani umeanza leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York ukibeba maudhui ya jumla juu ya changamoto na mafanikio ya utekelezaji wa malengo ya milenia hususan yale yanayohusu wanawake na wasichana. Taarifa zaidi na Assumpta Massoi.

(Taarifa ya Assumpta)

Mkutano ulianza kwa kumchagua Balozi Libran Cabactulan kutoka Ufilipino kuwa Mwenyekiti wa kamisheni hiyo itakayomaliza vikao vyake tarehe 21 mwezi huu, ikikutanisha wajumbe kutoka nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa wakiwemo mawaziri. Mwenyekiti akaweka bayana jukumu linalowakabili....

(Sauti ya Balozi Libran)

“Jukumu la kamisheni hii ni kutathminni mafanikio na maendeleo kwa wanawake na watoto kwa mujibu wa malengo ya milenia na kuweka bayana pengo lililopo na changamoto.”

Katibu Mkuu Ban Ki-Moon akaweka bayana kuwa safari ya kukomboa wanawake na wasichana barubaru imekuwa ndefu lakini hatua zimepigwa ikiwemo kujumuisha wavulana na wanaume katika kuhamasisha umuhimu wa usawa wa kijinsia, lakini bado kuna changamoto nyingi....

(Sauti ya Ban)

“Kumekuwepo na maendeleo kupunguza pengo la ajira kati ya wanawake na wanaume, lakini wanawake wako hatarini kupata ajira zisizokidhi, wakilipwa ujira mdogo, mazingira duni ya kazi bila mafao ya afya au pensheni na bila sheria za kazi zinazowalinda. Wanawake bado wanapata ujira mdogo kuliko wanawaume kwa kazi zinazofanana.”

Katibu Mkuu ametaka vitendo zaidi na sera za dhati za kuweka usawa wa kijinsia kuanzia majumbani, viwandani hadi kwenye vyumba vya mikutano kwani imedhihirika kuwa maeneo yenye usawa huo maendeleo ya jamii nzima yanakuwa dhahiri. Bwana Ban amesema yeye anaongoza kwa vitendo kwa kumteua Mary Robinson kuwa mwanamke wa kwanza kuongoza mashauriano ya amani.

Mkutano huo wa 58 wa kamisheni ya hali ya wanawake duniani utakuwa na vikao kadhaa ikiwemo kile kinachoangazia ukatili wa kijinsia kwenye ukanda wa maziwa makuu na mwelekeo wa jamii ukanda wa Sahel.