Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Haki ya kupiga kura kwa wanawake kutoka jamii za kiasili bado mashakani: Mshiriki wa CSW58

Haki ya kupiga kura kwa wanawake kutoka jamii za kiasili bado mashakani: Mshiriki wa CSW58

Wakati kikao cha 58 cha Kamisheni ya hali ya wanawake duniani kikiwa kinaendelea mjini New York,Marekani, washiriki kutoka taasisi za kiraia zinazotetea haki za wanawake wa jamii ya kiasili wamepaza sauti wakitaka madhila yanayokumba kundi hilo yaangaziwe na kupatiwa suluhu.

Beatrice Shanka kutoka taasisi ya Ilaramata huko Kajiado nchini Kenya ambaye amefadhiliwa na shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na wanawake, UN-Women, ametaja madhila yanayokumba wanawake hao wa jamii ya kimasai kuwa ni pamoja na kukiukwa kwa haki yao ya kupiga kura..

(Sauti ya Beatrice)

"Hali katika jamii yetu ni kwamba mara nyingi haki za wanawake zinapokwa!..Hususan inapokuja uchaguzi, wanawake hawapaswi kubeba vitambulisho vyao ya kupigia kura, na wanaume wanataka wanawake wapigie kura chaguo la mwanaume, jambo ambalo wanawake hawapendi. Pia ukeketaji unaoendelea, tunajitahidi kupiga vita kwani watu wengi kwenye jamii yetu wanaamini kuwa mwanamke asiyekeketwa si mwanamke halisi.”

Amesema hata wanapoamua kutetea haki hizo wanakumbwa na vikwazo ikiwemo kutengwa lakini hawakati tamaa kwa kuwa sasa wanaona Umoja wa Mataifa unatambua haki za jamii za kiasili na wanatumai kuwa nuru inaanza kuonekana.