Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mamilioni ya wanawake bado wanakabiliana na vikwazo kazini: ILO

Mamilioni ya wanawake bado wanakabiliana na vikwazo kazini: ILO

Shirika la Ajira Duniani, ILO, limesema kuwa wakati Siku ya Kimataifa ya Wanawake ikiadhimishwa hapo kesho Machi 8, wanawake bado wanakabiliwa na changamoto za kuwa na usawa kazini.

Shirika hilo limesema tangu lilipoanzishwa mnamo mwaka 1919, wanawake wengi duniani hawakuwa na haki ya kupiga kura, na wale wenye ajira walikuwa hawana fursa ya kutetea haki zao kwa sauti moja. Limesema sasa takriban karne moja baadaye, hatua zimepigwa kuhusu haki za wanawake kazini na wanawake wengi sasa wanafanya kazi.

Lakini, licha ya hatua hizo kupigwa, ILO imesema mamilioni ya wanawake bado wanakabiliwa na vikwazo vinavyozuia juhudi za kufikia usawa wa fursa na jinsi wanavyochukuliwa kazini. Katika ujumbe wake wa kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani mwaka huu, Mkurugenzi Mkuu wa ILO, Guy Ryder amemulika baadhi ya changamoto wanazokumbana nazo wanawake wanaofanya kazi, akisema kuwa kuwepo kwa wanawake katika nafasi za uongozi kazini kutasaidia kizazi kijacho cha wanawake kupanda ngazi ya ajira.