Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Guterres aelezea kushangazwa na viwango vya ukatili CAR

Guterres aelezea kushangazwa na viwango vya ukatili CAR

Kamishna Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi katika Umoja wa Mataifa, António Guterres, amesema kuwa mzozo uliopo sasa nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati si kitu kilichoibuka upya, kwani taifa hilo limekuwa likikumbwa na matatizo ya aina moja au nyingine kwa muda mrefu.

Bwana Guterres amesema hayo akilihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ambalo leo limekutana kujadili hali nchini humo. Amesema ulipofika mwaka 2012, tayari wakimbizi 165,000 kutoka CAR walikuwa wameandikishwa katika mataifa jirani ya Cameroon, Chad, DRC na Jamhuri ya Kongo, ingawa sasa idadi hiyo imepanda na kufikia wakimbizi 290,000, huku Cameroon ikitoa makao kwa idadi Kubra zaidi ya wakimbizi, ambayo ni 130,000 kwa ujumla.

 “Sikumbuki ziara yoyote niliyofanya katika miaka yangu 8 kama Kamishna Mkuu ambayo imenihuzunisha mno kama ile nilioifanya katika Jamhuri ya Afrika ya Kati. Nilishangazwa na ukatili na unyama ambao umekuwa sehemu ya machafuko yanayotendeka nchini humo na athari  zake kwa mateso wanayopata watu.”

Guterres amesema hali ni mbovu, huku wakimbizi wakiwasili wakiwa na uoga, utapiamlo, na wanyonge kabisa, baada ya kutembea na kujifisha mwituni kwa siku nyingi au wiki kadhaa. Misafara mingi inayoelekea mpakani inashambuliwa, huku vikosi vya kimataifa vikiwa vichache mno na bila uwezo wa kutoa ulinzi wa kutoasha.

“Wahudumu wa kibinadamu wanahangaika kuwahamisha wakimbizi kutoka maeneo walikotawanyika na ambayo ni magumu kuyafikia karibu na mpaka na kuwapeleka maeneo wanapoweza kupata usaidizi kabla ya msimu wa mvua. Lakini uwezo wetu kukidhi mahitaji yao yote ni mdogo kwani watu tunaowahudumia wamo katika hali mbaya mno, huku tukikabiliwa na kuongezeka changamoto na uhaba wa ufadhili”