Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Eliasson akutana na Kaimu Waziri wa Mambo ya nje wa Ukraine: Serry awasili Crimea

Eliasson akutana na Kaimu Waziri wa Mambo ya nje wa Ukraine: Serry awasili Crimea

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Jan Eliasson ambaye yuko nchii Ukraine hii leo amekuwa na mazungumzo na Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo Andrii Deshchytsia, mjini Keiv ambako wamejadili mzozo unaoendelea nchini humo.

Taarifa ya msemaji wa Umoja wa Mataifa imesema wawili hao wamesisitiza umuhimu wa utulivu na mshikamano wa kimataifa katika kusaka amani nchini humo.

Halikadhalika wamekubaliana kuwa njia zote za kidiplomasia zitumike zaidi kusaka amani. Bwana Eliasson amerejelea wito wa KAtibu Mkuu Ban Ki-Moon wa kutaka kuheshimiwa kwa mamlaka na utaifa wa Ukraine.

Wakati huo huo Roberty Serry ambaye ni mshauri mwandamizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amewasili kwenye jimbo linalojitawala la Crimea nchini Ukraine. Bwana Serry alitumwa na Katibu Mkuu kwenda eneo hilo kujionea hali halisi ilivyo na kisha ampatie taarifa.

Mzozo wa Ukraine umekuwa ukiimarika ambapo Umoja wa Mataifa umekuwa ukifanya jitihada kupatia suluhu ikiwemo vikao vya mwishoni mwa wiki vya Baraza la Usalama.