Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kampeni ya kuboresha miji duniani yazinduliwa hii leo:

Kampeni ya kuboresha miji duniani yazinduliwa hii leo:

Shirika la Umoja wa Mataifa la makazi ya watu, UN-HABITAT na wadau wake leo limezindua kijitabu ambacho ni dira ya aina ya miji inayotakiwa katika karne ya 21.

Uzinduzi wa kijitabu hicho umefanyika New York ikiwa ni sehemu ya kampni ya ushirikiano duniani ya kuboresha miji kuelekea mkutano wa saba wa majiji utakaofanyika huko Colombia mwezi ujao.

Mkurugenzi Mtendaji wa UN-HABITAT Dkt. Joan Clos amesema nyaraka hiyo inatoa mwongozo wa sera bora ambazo mamlaka za majiji zinaweza kufuata kwa ajili ya maendeleo endelevu ya maeneo hayo muhimu kwa uchumi wa nchi. Amesema sambamba na uzingatiaji wa misingi bora katika ujenzi wa miji, pia wanamulika uboreshaji wa maeneo ya makazi ya duni.

(Sauti ya Dkt. Clos)

Tunapaswa kubadili dhana ya usimamizi kwa kipindi hiki cha karne ya 21. Kwa sababu iwapo tutaendelea kuendeleza na kujenga miji kwa mtindo wa zamani, tutakuwa tunapanda mbegu ya kuendeleza janga la mabadiliko ya tabianchi, ukosefu wa maendeleo, ujumuishaji, utu na pia usimamizi mbovu unaoambatana na ubaguzi, umaskini na migogoro ya kijamii.”

UN-HABITAT inasema kuwa uendelezaji wa miji ni muhimu kwa kuwa asilimia 80 ya vipato vya kiuchumi duniani ni miji.