Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama lajadili ulinzi wa raia katika migogoro ya silaha

Baraza la Usalama lajadili ulinzi wa raia katika migogoro ya silaha

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, leo limefanya mjadala kuhusu ulinzi wa raia katika migogoro ya vita, likiangazia utekelezaji kikamilifu wa majukumu ya ulinzi wa raia wanaopewa wajumbe wa ulinzi wa amani. Joshua Mmali na taarifa kamili

(Taarifa ya Joshua)

Mjadala huo ambao ulipendekezwa na Uingereza, umewashirikisha maafisa wa ngazi za juu wa Umoja wa Mataifa, wakiwemo Mratibu Mkuu wa misaada ya kibinadamu na huduma za dharura, Valerie Amos na Mkuu wa Operesheni za Ulinzi wa Amani, Hervé Ladsous, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu, Navi Pillay, pamoja na Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu, Yves Daccordalso.

Wote katika hotuba zao wamesisitiza umuhimu wa pande zinazohasimiana katika migogoro kuheshimu na kuwalinda raia, wakimulika hali nchini Syria, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo na Sudan Kusini

Wa Kwanza kuzungumza, amekuwa Bi Navi Pillay, kupitia njia ya video

(NAVI PILLAY)

Kuna haja ya dharura yakukomesha ukatili katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, na kuwawajibisha wanaotekeleza uhalifu huo kisheria. Nafahamu kuwa afisi ya Mwendesha Mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ameamua kufungua uchunguzi. Narejelea pia wito wangu kwa Baraza hili kuipeleka kesi ya Syria kwa ICC, kama onyo kwa pande zote kuwa watawajibishwa kwa vitendo vyao”

Wa pili, Bi Valerie Amos

Raia wanaendelea kuuawa, kujeruhiwa, na kulemazwa katika mizozo kwa mashambulizi ya kulengwa au kiholela mara kwa mara. Wanalazimika kuhama bila kujua hatma yao, mara nyingi bila kupata mahitaji muhimu. Mifano ya hivi karibuni ya Syria, Jamhuri ya Afrika ya Kati na Sudan Kusini, inadhihirisha hili.”