Tarehe ya kusikiliza kesi dhidi ya Kenyatta huko ICC yasogezwa hadi itakapotangazwa

23 Januari 2014

Mahakama ya kimataifa ya uhalifu, ICC huko The Hague, Uholanzi, imefuta hadi itakapotangazwa tena, tarehe ya kuanza kusikilizwa kwa kesi inayomkabili Uhuru Kenyatta, kesi ambayo ilikuwa ianze tarehe Tano mwezi  ujao.

Hiyo ni kwa mujibu wa tangazo la lililotolewa leo na jopo la majaji wanaosikiliza sualahilolikiongozwa na Jaji Chile Eboe-Osuji.

Taarifa hiyo imesema badala yake tarehe hiyo mahakama itakuwa na kikao cha kusikiliza hali halisi ya masuala yaliyoibuliwa kwenye mchakato wa kesi hiyo kutoka upande wa mashtaka na ule wa utetezi.

Kikao hicho pia kitajumuisha pande husika na ombi la upande wa mashtaka la tarehe 12 mwezi uliopita la kutaka kuondolewa kwa baadhi ya mashahidi, ombi ambalo lilijibiwa kimaandishi na wawakilishi wa upande wa utetezi na wahanga wa ghasia za baada ya uchaguzi nchini Kenya mwaka 2007.

Bwana Kenyatta ambaye sasa ni Rais waKenya, anashtakiwa kwa makosa matano ya uhalifu dhidi ya binadamu ikiwemo kuhusika na mauaji, watu kuhama makwao kwa lazima, ubakaji na utesaji, mambo ambayo yanadaiwa kufanyika kati ya mwaka 2007 na 2008 baada ya uchaguzi mkuu.