Ni muhimu kujitoa ili kulinda mafanikio ya kiusalama mashariki mwa DRC: Kobler

13 Januari 2014

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limekutana leo kujadili hali katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, huku Mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo, MONUSCO akionya kuwa ni vyema kuendeleza kasi ya mafanikio yalopatikana kiusalama ili eneo la mashariki lisitumbukie tena katika mikono ya waasi. Joshua Mmali na taarifa kamili

TAARIFA YA JOSHUA

Akilihutubia Baraza hilo la Usalama, Mwakilishi wa Katibu Mkuu na Mkuu wa MONUSCO, Martin Kobler, amesema kuwa matukio ya kiusalama ya Disemba 30 mwaka ulopita, yalionyesha jinsi hali ilivyo dhaifu bado, na hivyo basi ni muhimu sasa hata zaidi kuendeleza kasi ya mafanikio yalopatikana kiusalama kufikia sasa.

Bwana Kobler amesema baada ya ushindi wa kijeshi dhidi ya waasi wa M23, ni muhimu sasa kuanza kutekeleza maazimio ya Nairobi. Amesema kuna ripoti za kuaminika kuwa usajili wa kijeshi wa M23 haukukoma baada ya maazimio ya Nairobi, na kwamba kuna vitendo vya M23 vinavyoibuka katika eneo la Ituri, kaskazini mashariki mwa DRC.

Natoa wito kwa serikali ya DRC kutekeleza maazimio ya Nairobi na kuharakisha harakati za kuwarejesha wapiganaji wa zamani wa M23 kaitika uraia. Wakati huo huo, natoa wito kwa serikali za Uganda na Rwanda kufanya kila ziwezalo ili kuzuia waasi wa M23 kujificha au kufanyia mafunzo ya kijeshi kwenye ardhi zao. Tusikubali kuibuka tena kijeshi kwa M23.

Bwana Kobler ametoa pia wito kwa jeshi la DRC kufanya juhudi zaidi katika mipango ya pamoja ya operesheni dhidi ya FDLR, na waasi wa Uganda wa ADF.

Baraza la Usalama pia limehutubiwa na Bi Mary Robinson, Mwakilishi Maalumu wa Katibu Mkuu katika ukanda wa Maziwa Makuu.