Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Utulivu watakiwa CAR baada ya viongozi wa mpito kujiuzulu:Babacar Gaye

Utulivu watakiwa CAR baada ya viongozi wa mpito kujiuzulu:Babacar Gaye

Huko Jamhuri ya Afrika ya Kati, Mwakilishi wa maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Jenerali Babacar Gaye ametaka utulivu nchini humo kufuatia kujiuzulu wa Rais Michel Djotodia na Waziri Mkuu wa serikali ya mpito Nicolas Tiangaye. Ametoa wito kwa wajumbe wa baraza la mpito kujikusanya na kufanya uchaguzi haraka wa mtendaji mpya wa mamlaka ya mpito kama ilivyokubaliwa wakati wa kikao kisicho cha kawaida cha wakuu wa Jumuiya ya kiuchumi ya nchi za afrika ya Kati, ECCA mjini N’Djamena Chad hapo jana. Jenerali Gaye ambaye ni mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuleta utulivu nchini humo, BINUCA ametoa wito kwa wananchi na viongozi kuwa na utulivu. Vikosi vya kimataifa ya kuleta amani nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, MISCA pamoja na vile vya Ufaransa vimepata maendeleo makubwa katika kuutwa tena mji mkuu Bangui. Amesema Umoja wa Mataifa na wadau wake wanaendelea kuhakikisha wananchi wapatao Milioni Mbili wanapatiwa misaada ya haraka wakati huu ambapo maelfu ya watu wamekimbia makazi yao na hata nje ya nchi kutokana na mapigano yanayoendelea nchini humo.