Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkuu wa UNMISS atembelea Malakal kujionea hali halisi

Mkuu wa UNMISS atembelea Malakal kujionea hali halisi

Takribani mwezi mmoja tangu kuanza kwa mapigano ya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan Kusini, mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, Hilde Johnson amefanya ziara ya kwanza kwenye mji mkuu wa jimbo la Upper Nile, Malakal, ili kujionea hali halisi.

Akiwa ziarani humo alitembelea eneo ambalo ujumbe wa Umoja wa Mataifa Sudan Kusini, UNMISS inahifadhi wakimbizi wa ndani 12,000 waliokimbia makwao kutokana na mapigano.

Bi. Johnson ambaye pia ni mkuu wa UNMISS alipata fursa ya kuzungumza na viongozi wa kijamii ambao pamoja na kuelezea hofu yao walitoa shukrani kwa Umoja wa Mataifa kwa usaidizi wanaopatiwa. Halikadhalika alifika hospitali inayotibu maelfu ya majeruhi wa mapigano hayo na kushuhudia kuzaliwa kwa watoto Kumi.

(Sauti ya Hilde)

"Kati ya wagonjwa 186 waliofika wakiwa na majeraha ya risasi wakati wa siku nne walizokumbwa na mapigano, ni mtoto mmoja tu ambaye alifariki duniani, wengine waliobakia maisha yao yaliokolewa.”

Huku akiwataka wananchi wa Sudan Kusini kuweka tofauti zao mbali na kusisitiza amani ametoa pongezi kwa wafanyakazi wa UNMISS huko Malakal ambao licha ya mazingira magumu na hatarishi, wamejitolea kuwahudumia wakimbizi hao waliosaka hifadhi eneo hilo.

Hadi sasa vituo kadhaa vya UNMISS nchini Sudan Kusini vinahifadhi takribani wananchi 60,000 huku zaidi ya wananchi Laki Mbili wakiripotiwa kupoteza makazi yao nchini humo tangu kuanza kwa mapigano.