Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sudan Kusini yazindua ushirika wa kulinda haki za watoto

Sudan Kusini yazindua ushirika wa kulinda haki za watoto

Shirika la Kuhudumia watoto katika Umoja wa Mataifa, UNICEF, limeipongeza serikali ya Sudan Kusini kwa kuanzisha shirikisho la wadau wa kulinda haki za watoto walio hatarini, ambalo ni la kwanza la aina yake nchini humo. Mwakilishi wa UNICEF nchini humo, Iyorlumun Uhaa, amesema kuwa watoto maskini zaidi na walio wanyonge zaidi katika nchi yoyote ile huwa hatarini, akisema kuwa kwa mkakati huo, watoto hao watalindwa ipasavyo.

UNICEF ilitoa usaidizi wa kitaaluma kwa Wizara ya Masuala ya Jinsia, Watoto, Maslai ya Kijamii na Masuala ya Kibinadamu katika kuliunda shirikisho hilo, ambalo linajumuisha viongozi wa ngazi ya juu Sudan Kusini, wakiwemo mawaziri wa zamani na wabunge.  Jukumu lake muhimu litakuwa ni kuishawishi serikali na kuisaidia wizara hiyo katika kuweka sera mwafaka za kuwalinda watoto walio hatarini.