Wanakandanda wa kimataifa Falcao kuwa balozi mwema wa UNODC:

20 Novemba 2013

Mkurugenzi mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na madawa na uhalifu UNODC Yury Fedotov, amemteuwa mwanasoka wa kimataifa kutoka Colombia Radamel Falcao García Zárate kuwa balozi mwema wa shirika hilo. Falcao, ni mshambuliaji hatari ambaye kwa sasa anaichezea timu ya Monaco F.C. baada ya kuondoka Atlético Madrid. Bwana Fedotov amesema Falcao amewika saana katika anga za kimataifa na atabeba matumaini ya taifa lake kwenye kombe la dunia hapo mwakani nchini Brazil.

Ameongeza kuwa mbali ya kupigania maslahi ya timu anayochezea kijana huyo ametumia ujuzi wake kuwachagiza vijana kwa kuwaonyesha njia ya kiafya ya kuishi sio tuu Colombia atokako bali duniani kote. Akizungumza baada ya uteuzi huo Falcao amesema anajivunia kuwa balozi mwema na lengo lake ni kuwasaidia vijana kote duniani kuyaonyesha mihadarati kadi nyekundu.

Falcao alianza mpira wa kulipwa mwaka 1999 akiwa na umri wa miaka 13 tuu na amefunga mabao zaidi ya 100 katika misimu mitatu ya soka barani Ulaya na hivyo kuwa mchezaji wa kwanza katika historia kushinda vikombe viwili mfululizo barani Ulaya katika timu mbili tofauti. Falcao amewekwa katika orodha ya kuwania Tuzo ya Puskás ya goli bora 2012 na tuzo ya FIFA Ballon d'Or 2012 na 2013.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter