OPCW yashinda tuzo ya amani ya Nobel: Ban apongeza

11 Oktoba 2013

Shirika la kimataifa la kupinga matumizi ya silaha za kemikali, OPCW limeshinda tuzo ya amani ya Nobel kwa mwaka huu wa 2013. Assumpta Massoi na taarifa kamili.

(Taarifa ya Assumpta)

OPCW lilikuwa miongoni mwa majina 259 yaliyowasilishwa kuwania tuzo hiyo ambapo shirika hilo ambalo kwa sasa linasimamia uteketezaji wa mpango wa silaha za kemikali wa Syria, limeibuka mshindi.

Mkurugenzi Mkuu wa OPCW Ahmet Üzümcü punde baada ya kupata taarifa hizo alishindwa kuficha hisia zake na kusema kuwa kila wakati walikuwa wanatambua kuwa kazi yao inaleta amani duniani kimya kimya lakini kwa uhakika. Amesema wiki chache zilizopita zimeweka hilo bayana na kwamba Jumuiya nzima ya kimataifa imetambua kazi yao.

Üzümcü amesema ni heshima kubwa kwake yeye na watendaji wenzake lakini bila ushirikiano kutoka nchi husika kazi hiyo isingaliwezekana. Corinne Momal-Vanian kutoka ofisi za Umoja wa Mataifa Geneva, anazungumzia tuzo hiyo.

(Sauti ya Corinne)

“Umoja wa Mataifa unakaribisha ushindi huo wa tuzo ya amani ya nobel kwa OPCW. Inadhihirisha kazi ya shirika hilo kwa ushirikiano na Umoja wa Mataifa ya kutokomeza silaha za kemikali ikiwemo nchini Syria,kazi inayofanywa katika mazingira magumu.”

Akizungumzia ushindi huo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon ametoa pongezi akisema umekuja karibu miaka 100 baada ya shambulio ka lwanza la silaha za kemikali na kwamba OPCW imeimarisha uzingatiaji sheria kwenye matumizi ya silaha za kemikali.

Miongoni mwa waliokuwa wakiwania tuzo hiyo ya amani ya Nobel ni mtoto wa kike Malala Yousfzai aliyepigwa risasi na watalibani kutokana na kutetea elimu ya mtoto wa kike nchini Pakistani, na Daktari wa wanawake kutoka DR Congo, Denis Mukwege.