Mkataba wa Minamata kuhusu Zebaki waanza kutiwa saini: UNEP

9 Oktoba 2013

Hatimaye mkataba wa kimataifa wa kuzuia matumizi ya zebaki umefunguliwa rasmi Jumatano nchini Japan kwa serikali kuanza kutia saini na hivyo kudhihirisha kuanza kwa kipindi muhimu cha jitihada za kudhibiti matumizi ya Zebaki ambayo ni sumu na hatari kwa maisha ya viumbe hai pamoja na mazingira. Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la mazingira duniani, UNEP Achim Steiner amesema hatua ya leo ni muhimu baada ya miaka minne ya mashauriano na kwamba kupitia mkataba huo mataifa yameweka misingi ya hatua za kuchukuliwa kimataifa iwapo uchafuzi kupitia madini hayo utabainika. Amesema mkataba huo una manufaa kwa kila mtu duniani hususan wafanyakazi na familia za wachimbaji wadogo wadogo wa madini atanufaika na uwepo wake.  Mathalani mkataba unaweka udhibiti na upunguzaji wa matumizi ya madini ya zebaki katika vifaa tiba na hata kwenye sekta ya uchimbaji madini na viwanda vya saruji. Kwa mujibu wa UNEP, madhara ya kiafya yatokanayo na matumizi ya Zebaki ni pamoja na kuharibu ubongo na mfumo wa mishipa ya fahamu hususan miongoni mwa vijana pamoja na figo. Mkataba huo ulipatiwa jina la MINAMATA ambao ni mji mmoja nchini Japan uliokumbwa na uchafuzi wa zebaki na kusababisha madhara ya kiafya karne iliyopita.