Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mratibu wa masuala ya kibinadamu alaani mauaji ya watoa misaada CAR:

Mratibu wa masuala ya kibinadamu alaani mauaji ya watoa misaada CAR:

Mratibu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa huko Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) Kaarina Immonen, amelaani vikali mauaji ya wafanyakazi wawili wa misaada wa ACTED mjini Bossangoa mwishoni mwa wiki.  Bi Immonen ametoa salamu za rambirambi kwa familia na marafiki wa wafanyakazi hao na kwa wafanyakazi wote wa ambao hujitolea bila kuchoka kutoa msaada na ulinzi kwa watu wanaohitaji msaada huko CAR. Amesema inashtusha kuona wafanyakazi wa misaada wanalengwa na ametaka mauaji kamahayo yalaaniwe kwa kila njia. Ameutaka uongozi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati na pande zote zinazohusika kwenye vita kuhakikisha ulinzi kwa raia na kuheshimu sheria za kimataifa za haki za binadamu, pamoja na watoa misaada. Ameongeza kuwa kuendelea kutokuwepo kwa usalama, kutokuwepo kwa utawala wa sheria, ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na mashambulizi dhidi ya watoa misaada na vifaa vyao vinazuia msaada wa kuokoa maisha kuwafikia walengwa. Mwezi Agosti pekee mapigano Kaskazini Magharibi mwa nchi yamesababisha vifo 148 na kuwafungisha virago watu 4100 waliokimbilia Chad, huku zaidi ya 17,000 wamelazimika kuwa wakimbizi wa ndani.