Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kujua kusoma na kuandika kwa wote bado ni ndoto:UNESCO

Kujua kusoma na kuandika kwa wote bado ni ndoto:UNESCO

Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na Elimu, Sayansi na Utamaduni UNESCO, limetoa ripoti ambayo inasema Zaidi ya asilimia 84 ya watu wazima ambao walikuwa wahajui kusoma na kuandika sasa wanaweza kufanya hivyo kiwango hicho ni ongezeko la asilimia 8 katika kipindi cha kuanzia mwaka 1990.

Hata hivyo UNESCO inasema kuwa bado kuna watu milioni 774 duniani kote ambao hawajui kusoma na kuandika.

Takwimu hizo mpya ambazo zimetolewa kuambatana na siku ya kujua kusoma duniani inayoadhimishwa kila Septemba 8, inaonyesha kuwa idadi kubwa ya watu wanaokabiliwa na tatizo hilo wanaishi baraniAsia  na Afrika.

Barani Asia pekee wengi wako katika maeneo ya Kusini na Kaskazini na idadi kubwa nyingine inapatikana katika eneo la Kusin mwa Sahara.

Takwimu zinaonyesha kuwa, robo tatu ya wale wasiojua kusoma na kuandika ni wanawake na kwamba hali hiyo inaweza kuongezeka hata wakati wa kufikiwa tarehe ya mwisho ya malengo ya maendeleo ya milenia ambayo ni mwaka 2015.

Katika ujumbe wake kuadhimisha siku hii, Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO Irina Bokova ametoa wito wa kuboreshwa kwa hali ya elimu kwani bila kufanya hivyo kunaweza kusababisha dunia kurudi nyuma kimaendeleo.