Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Malala azindua ombi la elimu, asema walioshambulia wanafunzi Pakistani ni waoga na wanahaha

Malala azindua ombi la elimu, asema walioshambulia wanafunzi Pakistani ni waoga na wanahaha

Binti wa kike aliyenusurika shambulio la bomu lililofanywa na watalibani dhidi yake na wanafunzi wengine miezi Minane iliyopita huko Pakistani amewaita walioshambula kwa mabomu wanafunzi huko Quetta, Pakistani siku ya Jumamosi kuwa ni waoga na wanahaha kuwanyima watoto wa kike haki yao ya elimu. Malala Yousfzai ambaye kwa sasa anaishiBirmingham, Uingereza ametoa kauli hiyo baada ya kuwa mtu wa kwanza kutia saini ombi la dharura duniani linalotaka hatua za haraka za kuhakikisha kila mtoto wa kike anakwenda shule. Ombi hilo linaloungwa mkono na Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa Gordon Brown litawasilishwa na Malala mwenyewe kwenye Umoja wa Mataifa tarehe 12 mwezi ujao, tarehe ambayo binti huyo atakuwa anatimiza umri wa miaka Kumi na Sita. Takwimu zaonyesha kuwa watoto Milioni 57 duniani kote wa kike na wa kiume hawaendi shule kutokana na sababu mbali mbali na hivyo Malala anataka hatua zaidi ikiwemo ujenzi wa shule kuwezesha watoto kwenda shuleni.