Guinea Bissau na Mashariki ya Kati zaangaziwa katika Baraza la Usalama

22 Mei 2013

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, leo limefanya vikao viwili: cha kwanza kuhusu hali nchini Guinea Bissau na cha pili kuhsu hali Mashariki ya Kati. Joshua Mmali ana maelezo zaidi.

(TAARIFA YA JOSHUA)

Katika kikao chake kuhusu hali nchini Guinea Bissau, Baraza la Usalama kwa kauli moja limepitisha azimio la kuongeza muda wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo kwa kipindi kingine cha miezi 12, hadi Mei 31 mwaka 2014, ili usaidie katika kutoa huduma muhimu kabla na baada ya uchaguzi.

Azimio hilo pia limeamuru uundaji wa jopo la wataalam watakaosaidia katika kukabiliana na ulanguzi wa madawa ya kulevya nchini humo.

Kura ya kupitisha azimio hilo imefuatia ripoti ya Katibu Mkuu ilowasilishwa kwa Baraza la Usalama kuhusu hali nchini humo, zikiwemo juhudi za kurejesha utaratibu wa kikatiba.

Kuhusu hali Mashariki ya Kati, Baraza la Usalama limesikiliza ripoti ya Mwakilishi wa Katibu Mkuu na Mratibu Maalum wa harakati za amani Mashariki ya Kati, Robert Serry. Bwana Serry amesema hali Mashariki ya Kati bado ni tete, inageuka baa la kibinadamu, na hali ya baadaye haifahamiki.

Kumaliza mzozo wa Syria ni suala la dharura na ni lazima liwe la suala la kipaumbele kwa jamii ya kimataifa. Wakati huo huo, litakuwa kosa kubwa na hatari kudhani kuwa kuutatua mzozo baina ya Waisraeli na Wapalestina hakuna umuhimu mkubwa. Huu sio wakati wa kulegeza ahadi zetu za kuendeleza matumaini ya kurejelea mazungumzo ya amani, ili kufikia suluhu la kuwepo mataifa mawili huru. Huu ndio wakati wa juhudi za pamoja, kuunga mkono mkakati uliopo sasa, ili tusipoteze fursa kubwa iliyowekwa hivi karibuni.”