Kila kizazi na kifo kihesabiwe:Wito kutoka Bangkok

19 Aprili 2013

Mkutano wa kwanza wa kimataifa kuhusu usajili wa umma na takwimu muhimu zinazohitajika umemalizika huko Bangkok Thailand ambapo serikali, mashirika ya Umoja wa Mataifa na yale ya maendeleo yametoa wito kwa nchi zote duniani kuhakikisha matukio muhimu kama uzazi na kifo pamoja na sababu za kifo yanasajiliwa.

Washiriki wamesema hatua hiyo ni muhimu kwani itawezesha nchi husika na washirika kupata misaada stahili ya kisiasa na kiufundi kulingana na mazingira husika na hata kupanga vyema mipango ya baadaye.

Kuboresha mfumo wa usajili wa takwimu za umma ni muhimu ili kuimarisha mifumo ya afya, kauli ya Dkt Marie-Paul Kieny kutoka WHO akifafanua kuwa ukifahamu idadi ya watoto waliozaliwa, watu wangapi wamefariki dunia na sababu za msingi za vifo inakuwa rahisi zaidi kuweka vipaumbele vya afya.

Afisa kutoka Tume ya Uchumi ya Afrika Abdalla Hamdock amesema kwa bara la Afrika nchi nyingi zinahaha kuandaa mifumo ya usajili wa takwimu muhimu na hivyo tume hiyo na washirika wake wanasaidia nchi hizo katika maandalizi hayo.