Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Syria yaripotiwa kugomea uchunguzi, Ban azungumza

Syria yaripotiwa kugomea uchunguzi, Ban azungumza

Wakati maandalizi ya jopo tangulizi la kuchunguza madai ya matumizi ya silaha za kemikali nchini Syriayakiwa yamekamilika, imedaiwa kuwa serikali ya Syria haikubaliani na muundo na mfumo wa uchunguzi huo. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon ambaye aliunda jopohilo, alipoulizwa na waandishi wa habari mjini Vatican kuhusu taarifa hizo amesema hajapata mawasiliano rasmi kutoka serikali ya Syria. Hata hivyo amesema inasikitisha ya kwamba Syria haijakubaliana na muundo aliopendekeza wa kutuma ujumbe kuchunguza madai ya matumizi ya silaha za kemikali nchini Syria. Bwana Ban amerejelea kauli yake kuwa uamuzi wa kupeleka ujumbe huo unafuatia madai yaliyowasilishwa na serikali ya Syria tarehe 20 mwezi uliopita na pia kutoka Uingereza na Ufaransa tarehe 21 mwezi huo huo. Katibu Mkuu amesema wakati huu ambapo jopo hilo liko Cyprus tayari kuelekea Syria, ameisihi serikali ya Syria kuruhusu uchunguzi huo uendelee na itoe ushirikiano wa kutosha.