Mkataba wa kudhibiti biashara ya silaha wakwama, Ban asikitishwa

29 Machi 2013

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon ameeleza kusikitishwa kwake na kitendo cha wajumbe mkutano wa mwisho wa mkataba wa kimataifa wa biashara ya silaha duniani kushindwa kuafikiana juu ya rasimu ya mkataba huo. Katika taarifa iliyotolewa na msemaji wa Katibu Mkuu siku ya Alhamisi ambayo ilikuwa siku  ya mwisho ya mashauriano hayo mjini New York, Marekani, Bwana Ban amesema kulikuwepo na viashiria ya kwamba mkataba huo ungaliridhiwa. Amesema aliamini kuwa rasimu ya mkataba ilikuwa imegusa pande zote na kwamba ingaliweza kuweka viwango thabiti vya pamoja vya kudhibiti biashara ya silaha duniani. Bwana Ban amesema ni matumaini yake kuwa nchi hizo zitaangalia njia zote za kuwezesha mkataba huo kupitishwa. Katika taarifa yake Bwana Ban hata hivyo amemshukuru Mwenyekiti wa mkutano huo Balozi Peter Woolcott, kwa kile alichoelezea ni uongozi wake thabiti wakati wa mashauriano bila kusahau mashirika ya kiraia na idadi kubwa ya nchi kwa kuunga mkono suala hilo. Kwa takribani wiki mbili wawakilishi kutoka serikali, mashirika ya kimataifa na kikanda pamoja na mashirika ya kiraia walifanya mashauriano ya mwisho kuhusu mkataba huo. Mashauriano hayo yanafuatia mkutano wa aina hiyo wa mwezi Julai mwaka jana ambapo pia wajumbe walishindwa kufikia muafaka.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud