Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ofisi za UM Bangui zaporwa: OCHA

Ofisi za UM Bangui zaporwa: OCHA

Kutokana na hali ya usalama kuwa tete huko Jamhuri ya Afrika ya Kati, Umoja wa Mataifa umesema utawaondoa wafanyakazi wake wasiohitajika kutoka  mji mkuu Bangui baada ya waasi kutwaa mamlaka ya nchi hiyo.  Watakaohamishwa watapelekwa kwenye makao ya muda mjini Yaounde nchini Cameroon. Ofisi za mashirika kadha ya Umoja wa Mataifa zimeporwa na vifaa kuharibiwa huku misaada ikiibia. Amy Martin kutoka ofisi ya Shirika la kuratibu masuala ya kibinadamu la Umoja wa Matafa OCHA anaitaja hali mjini Bangui kama isiyotabirika.

Anasema hata baada ya hali ya hatari kutangazwa bado milio ya risasi inasikika kwenye vitongoji vya mji huo.

(SAUTI AMY)

“Si salama kuendelea kuhudumu, hamna aliye na mahala pa kuishi , hamna aliye na umeme, hamna aliye na maji na hamna aliye na ofisi ya kufanyia kazi kila kitu kimeporwa. Ofisi ya Umoja wa Mataifa imeporwa, baadhi ya maghala yao yameporwa hata kama si yote. Kwa sasa tuna UNHCR, UNFPA,UNDP na ninaamini UNAIDS. Usalama ni jambo muhimu, tunajiondoa kwenye madhara. Tuna matumaini hali itatulia hivi katibuni, lakini kama itaendelea hivi hapana, hali haitakuwa salama kwa wafanyikazi wa kibinadamu kufanya kazi jinsi yunavyotaka. Tunajaribu kutuma wafanyikazi wetu wasiohitajika na famiia zao kwenda kwa uwanja wa ndege ili  wapate kusafirishwa kwenda Younde. “

Afisa huyo wa OCHA amesema hali ya kibinadamu kwa takriban watu Milioni Moja na Nusu wanaohitaji msaaada kwenye Jamhuri ya Afrika ya Kati itakuwa mbaya ikiwa hakutakuwa na utulivu na watoa misaada kuruhusiwa kuwafikia wanaohitaji msaada.