Matumaini ya udhibiti wa biashara ya silaha yaelekekezwa New York.

18 Machi 2013

Mkutano wa mwisho wa Umoja wa Mataifa kuhusu mkataba wa kimataifa wa biashara ya silaha umeanza mjini New York, Marekani ambapo Katibu Mkuu Ban Ki-Moon ametaka washiriki wa mkutano huo kujikita katika kuangalia madhara yatokanayo na biashara hiyo ambayo amesema ni vyema ikawekewa udhibiti.  Katika hotuba yake kwa washiriki wa mkutano huo utakaomalizika tarehe 28 mwezi huu, Bwana Ban amesema biashara zote duniani zina mbinu za kudhibiti kuanzia zile za vyakula, wanasesere na hata samani na akahoji kwa nini hiyo ya silaha kuna kigugumizi  cha kuweka viwango.  Bwana Ban amesema katika nchi za Amerika Kusini magwiji wa biashara za dawa za kulevya wanamiliki silaha nzito hata kuzidi majeshi  ya serikali zao na inashindwa kufahamika silaha hizo wanazipata kutoka wapi. Amesema mkutano huo uwe ni fursa ya kuweka ukomo ili kuondoa machungu yatokanayo na matumizi holela ya silaha yatokanayo na biashara holela.

(SAUTI YA BAN)

“Mkataba thabiti wa biashara ya silaha utahitaji nchi zinazouza silaha kutathini athari za matumizi ya silaha hizo katika ukiukwaji wa haki za binadamu au kuchochea migogoro. ATT itawaweka bayana wababe wa kivita, wakiukaji wa haki za binadamu, vikundi vya uhalifu, magaidi na watumiaji holela wa silaha. “

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud