Kila mtoto ana haki ya kupata huduma bora ya afya: UM

7 Machi 2013

Kamishina mkuu wa haki za binadfamu kwenye Umoja wa Mataifa Navi Pillay amesema haki ya afya ni haki ya msingi ya binadamu inayotambuliwa na mkataba wa kimataifa wa mtoto ambao unataka kila nchi ichukue hatua kupunguza vifo vya watoto na kufutilia mbali mambo yoyote yanayomdhuru mtoto.  Akizungumza kwenye baraza la haki za binadamu huko Geneva ambalo limejadili haki za mtoto, Pillay amesema kuwa Watoto Milioni Sita Nukta Tisa kote duniani wanakufa kila mwaka kabla ya kutimiza umri wa miaka Mitano.  Amesema hatari inayowakabili watoto kufariki dunia kabla ya kutimiza umri wa miaka  mitano kwenye nchi zinazoendelea ni mara 18 zaidi  ya nchi zilizostawi. Halikadhalika kumeripotiwa kuongezeka kwa visa vya matatizo ya akili miongoni mwa vijana barubaru. Pillay anasema kuwa kuna makundi ya watoto wanaotaabika hususan wale walio walemavu, watoto wahamiaji , walio vituoni bila ya uangalizi wa wazazi na waathiriwa wa mizozo na pia wale wanaodhulumiwa kimapenzi.

(SAUTI YA PILLAY)

 

“Kila saa watoto 300 wanakufa kutokana na utapiamlo, ambao pia hutatiza ukuaji wa takriban watoto milioni 170 kote duniani. Hili halikubaliki na hatua za mapema ni lazima zichukuliwe kulinda haki za watoto wote kuishi na kukua. Kando na tatizo la magonjwa na kukosa kukua yote yanayotokana na lishe duni, uzito kupita kiasi miongoni mwa watoto ni jambo linaloendela kutia wasi wasi. Mwaka 2010 kulikuwa na takriban watoto milioni 42 chini ya miaka mitano waliokuwa na uzito wa kupita kiasi na idadi hii inazidi kuongezeka kutokana na ukosefu wa mazoezi na lishe duni.”