Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uhusiano kati ya mazingira na haki za binadamu ni dhahiri

Uhusiano kati ya mazingira na haki za binadamu ni dhahiri

Mtaalamu huru wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu na mazingira, John Knox amesema kuna umuhimu wa haraka wa kufafanua ni jinsi gani haki za binadamu zinahusiana na kufurahia mazingira safi, huru na salama.

Katika ripoti yake mbele ya Baraza la haki za binadamu, Knox amesema ufafanuzi huo ni muhimu ili serikali na taasisi zingine ziweze kuelewa wajibu wao ni upi na kuhakikisha kuwa wanausimamia kuanzia ngazi ya kitaifa hadi kimataifa.

Amesema haki za binadamu na mazingira siyo tu vinahusiana bali pia vinategemeana na hivyo mazingira salama ni jambo la msingi kwa mtu kuweza kufurahia haki za binadamu na halikadhalika utekelezaji wa haki za binadamu ni muhimu kwa ajili ya mazingira salama.

Mathalani amesema serikali zinapaswa kutambua kazi nzuri zinazofanywa na watetezi wa haki za binadamu kuhusu masuala ya ardhi na mazingira wanapojaribu kuweka mizania ya maendeleo ya kiuchumi na uhifadhi wa mazingira.

Mtaalamu huyo amesema haki zote za binadamu ziko hatarini kutokana na uharibifu wa mazingira na hivyo basi ili haki za binadamu ziweze kusimamiwa ni lazima kuwepo na mazingira bora.