Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR yataka hatua zichukuliwe kuzuia ajali za boti kwenye Bahari ya Hindi

UNHCR yataka hatua zichukuliwe kuzuia ajali za boti kwenye Bahari ya Hindi

Shirika la Kuhudumia Wakimbizi katika Umoja wa Mataifa, UNHCR, limeelezea kusikitishwa na kuongezeka kwa idadi ya watu wanaokufa kwenye Bahari Hindi wakati wakikimbilia usalama wao na kutafuta maisha bora katika nchi za kigeni.

Kwa mujibu wa UNHCR, wengi wao ni watu wa jamii ya Rohingya kutoka jimbo la Rakhine, Myanmar, na wengine wakitoka kutoka kwenye kambi za wakimbizi, Bangladesh. Mnamo mwaka 2013, maelfu ya watu wanakadiriwa kuwa wamepanda boti za kimagendo, wengi wao wakiwa ni wanaume, ingawa pia kuna ripoti nyingi za wanawake na watoto kupanda boti hizi duni na hatari. Andrej Mahecic ni msemaji wa UNHCR

(SAUTI YA ANDREJ MAHECIC)

“Tunakadiria kuwa, miongoni mwa watu 13,000 walioondoka kwa boti za magendo mwaka 2012, takriban watu 500 walifariki dunia baharini boti hizi zilipoharibika au kuzama. Ni dhahiri kuwa Bahari Hindi imekuwa eneo la hatari zaidi duniani kwa watu wanaokimbia nchi zao. Katika kisa cha hivi karibuni kabisa wiki moja ilopita, watu 90 wanaoaminika kuwa wa jamii ya Rohingya, wameripotiwa kufa kutokana na kiu na utapia mlo wakati wa safari ya takriban miezi miwili.”