Baraza la usalama lipaze sauti moja kulinda raia kwenye migogoro

12 Februari 2013

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limekumbushwa jukumu lake la kupaza sauti moja ili kulinda maisha ya raia wasio na hatia wanaojikuta katikati ya mizozo sehemu mbali mbali duniani.

Hayo yameibuka wakati wa mjadala wa wazi kuhusu usalama wa raia kwenye maeneo ya migogoro ambapo Kamishna Mkuu wa tume ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa Navi Pillay amesema kila wakati kunaweza kuwepo kutokukubaliana juu ya hatua za kuchukua dhidi ya jambo fulani.

Hata hivyo amesema pindi   maisha ya mamia ya maelfu ya raia yanakuwa hatarini kama ilivyo huko Syria na kwingineko, dunia inatarajia Baraza la Usalama liungane na kuchukua hatua.

Ameeleza kuwa idadi ya raia waliouawa nchini Syria tangu kuanza kwa vuguvugu dhidi ya Rais Bashar Al Assad mapema mwaka 2011 huenda sasa inafikia Elfu Sabini na kwamba kutokukubaliana ndani ya Baraza la Usalama kunaibua janga linaloshuhudiwa sasa.

Mapema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon alieleza kuwa utu wa binadamu unazidi kukandamizwa kwenye maeneo ya migogoro lakini akakumbusha kuwa wajibu wa kulinda raia hauko mikononi mwa pande zinazopingana kwenye mzozo huo bali kwa kila mtu.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter