Elimu jumuishi kwa watoto wenye ulemevu yabadilisha maisha: UNICEF

7 Februari 2013

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limesema sera endelevu kuhusu elimu jumuishi kwa watoto wenye ulemavu imekuwa na mafanikio makubwa katika nchi za Ulaya ya Kati na Mashariki pamoja na Asia ya Kati.

Hayo yamebainika katika kikao cha bodi ya utendaji ya UNICEF mjini New York, Marekani kilichojikita kwenye masuala ya watoto wenye ulemavu.

Washiriki walipatiwa mfano wa Serbia ambako chini ya programu ya elimu jumuishi shule nyingi zinaandikisha darasa la kwanza watoto wenye ulemavu,  na kwamba kampeni za kitaifa za aina hiyo huko Montenegro zikijumuisha vyama vya kiraia zimezaa matunda kwa kuwa hata umma sasa unataka elimu jumuishi.

Mwenyekiti wa bodi ya UNICEF ambaye pia ni mwakilishi wa kudumu wa Finland kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Jarmo Viinanen, alifafanua kuwa elimu jumuishi haihitaji shule maalum na malezi maalumu bali kila mtoto bila kujali ulemavu alio nao, jinsia, kipato, dini  anaweza kwenda shule yoyote jirani na nyumbani kwake itakayomwezesha kuibua vipaji vyote alivyo navyo.

UNICEF inasema elimu jumuishi inaongeza zaidi utengamano, kuvumuliana na kujenga usawa katika jamii baina ya watoto wote badala ya kuwatenga wale walio na ulemavu.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud