Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mali na Syria zatawala hotuba ya Ban huko Davos

Mali na Syria zatawala hotuba ya Ban huko Davos

Hali ya amani nchini Mali na Syria zinazidi kuzorota na hivyo tuchukue hatua haraka kwa pamoja, na huo ndio ujumbe wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon kwa viongozi mbali mbali wa dunia wanaohudhuria jukwaa la uchumi huko Davos Uswisi.

Katika hotuba yake Ban amesema migogoro hiyo inahatarisha usalama siyo tu wa nchi hizo bali pia maeneo jirani na dunia nzima huku raia wasio na hatia wakiendelea kupoteza maisha, wengine kupoteza makazi na watoto kushindwa kwenda shule.

Ametoa mfano wa Mali ambapo amesema nchi hiyo iko kwenye kitisho kikubwa kutoka kwa waasi na vikundi vyenye silaha na msimamo mkali.

Bwana Ban amesema umaskini uliokithiri, hali mbaya ya hewa, taasisi dhaifu na usafirishaji wa dawa za kulevya na upatikanaji holela wa silaha nzito nchini humo vinaongeza zaidi madhila na ukosefu wa usalama ndani na nje ya nchi hiyo.

Kuhusu Syria amesema mgogoro huo wenye chimbuko lake la kisiasa unazidi kupanuka na ametaka nchi zote zinazopatia silaha pande husika kwenye mgogoro huo uliosababisha vifo vya watu zaidi ya Elfu Sitini, ziache mara moja. Amesema suluhisho la mgogoro huo ni la kisiasa na si vinginevyo.

Bwana Ban amesema Umoja wa Mataifa utaendelea na jitihada zake za kupatia suluhu migogoro hiyo.