Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban afanya mashauriano na waziri wa mambo ya nje wa Uturuki

Ban afanya mashauriano na waziri wa mambo ya nje wa Uturuki

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, leo amekutana na kufanya mashauriano na waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Bwana Ahmet Davutoğlu mjini Davos, Uswisi, ambako kongamano la kimataifa kuhusu uchumi linaendelea.

Bwana Ban na Waziri Davutoğlu wamebadilishana mawazo kuhusu mzozo wa Syria, na uwezekano wa suluhu la kisiasa. Katibu Mkuu ameelezea shukran zake kwa ukarimu wa Uturuki, kwa kuwakaribisha na kuwapa makazi wakimbizi wa Syria, tangu mzozo ulipoanza.

Aidha, Bwana Ban ameipongeza Uturuki kwa msaada wake kwa Somalia, hususani katika sekta ya usalama. Wawili hao pia wamezungumzia hali ya Iraq na matumaini ya mazungumzo ya Cyprus kurejelewa, pamoja na juhudi za amani Mashariki ya Kati na hali nchini Mali.