AFISMA wanahitaji vifaa haraka: Feltman

22 Januari 2013

Msimamizi mkuu wa masuala ya kisiasa ndani ya Umoja wa Mataifa Jeffrey Feltman amesema kwa kuwa tayari maafisa na askari wanaounda jeshi la Afrika huko Mali, AFISMA  wameanza kuwasili nchini humo, kinachotakiwa hivi sasa ni usaidizi haraka wa vifaa ili waweze kukabiliana na hali halisi.

Feltman amesema hayo wakati akitoa taarifa ya  hali ilivyo huko Mali mbele ya Baraza la usalama lililokuwa na mjadala wa wazi kuhusu Mali wakati huu ambapo operesheni za anga na za ardhini zinaongozwa na Ufaransa kuwafurumusha vikundi vyenye silaha kaskazini mwa nchi hiyo.

Amesema hadi tarehe 20 mwezi huu AFISMA ilikuwa na askari 855 kutoka Benin, Nigeria, Senegal na Togo na kwamba imekubalika kuwa idadi ya watendaji iongezwe na kufikia 3,300 ili kuweza kuimarisha operesheni dhidi ya vikundi vyenye silaha.

((SAUTI YA FELTMAN)

 Feltman anasema kuwa uwezo wa vikundi vyenye silaha vinavyoshikilia maeneo ya kaskazini mwa Mali umethibitika kuwa ni mkubwa kwa kuwa wanavifaa na wana ufundi kuliko ilivyotarajiwa.

Halikadhalika amesema Umoja wa Afrika na Jumuiya ya uchumi ya nchi za Magharibi mwa Afrika, ECOWAS zinakamilisha orodha kamilifu ya mahitaji ambayo itawasilishwa kwenye mkutano wa Umoja wa Afrika utakaofanyika tarehe 29 mwezi huu huko Addis Ababa Ethiopia.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter