Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Masuala ya Afrika kuendelea kumulikwa Baraza la Usalama

Masuala ya Afrika kuendelea kumulikwa Baraza la Usalama

Harakati za kupatia suluhu migogoro mbali mbali inayoendelea barani Afrika zitaendelea katika baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa mwezi huu wa Januari, na hiyo ni kwa mujibu wa Rais wa  kipindi hicho Balozi Masood Khan kutoka Pakistani.

Akitangaza mpango wa kazi wa Baraza la Usalama mbele ya waandishi wa habari mjini New York, Marekani hii leo, Balozi Khan amesema mpango huo wa awali umeridhiwa na wajumbe wa Baraza la Usalama ambapo pamoja na masuala ya Afrika pia kutakuwepo na mjadala kuhusu mikakati ya kukabiliana na ugaidi duniani na mbinu za kuboresha operesheni za kulinda amani za Umoja wa Mataifa.

Taarifa na mashauriano yamepangwa kuhusu Jamhuri ya Afrika ya kati na pia tutaangalia uongezaji wa muda wa kazi wa ofisi ya Umoja wa Mataifa huko Jamhuri ya Afrika ya Kati ambao unamalizika mwishoni mwa mwezi huu. Halikadhalika hali ilivyo kati ya Sudan na Sudan Kusini, na pia tutapata taarifa kutoka ofisi ya umoja wa mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu kuhusu hali ya kibinadamu kwenye majimbo ya Kordofan kusini na Blue Nile.”