Rushwa ni kikwazo kwa malengo ya milenia, kila mtu aikatae na aifichue: Ban

9 Disemba 2012

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon, amesema kadri ambavyo nchi zinajizatiti kufikia malengo ya maendeleo ya milenia suala la kupambana na rushwa linakuwa ni la muhimu kuliko wakati wowote.

Amesema hayo katika ujumbe wake wa siku ya kupambana na rushwa hii leo tarehe Tisa Disemba na kusema kuwa gharama ya rushwa inathibitishwa siyo tu kwa mabilioni ya pesa yanayofujwa, bali kwa taswira ya kutokuwepo kwa hospitali, shule, maji safi na salama, barabara, madaraja na kadhalika.

Bwana Ban amesema rushwa inatokomeza fursa na kujenga matabaka huku ikikiuka haki za binadamu, utawala bora na kudidimiza ukuaji wa kiuchumi.

Kwa mantiki hiyo ametaka nchi zaidi kuridhia mkataba wa kimataifa wa kupambana na rushwa ambao hadi sasa ni nchi 164 tu zimeridhia na kuongeza kuwa katika kuadhimisha siku hii, kila mtu ajitahidi ili rushwa iweze kukataliwa na kufichuliwa na hivyo kuwezesha mamilioni ya watu kutimiza ndoto zao za ustawi.