Mgogoro Sahel kuwa sehemu ya ajenda ya Baraza la Usalama UM mwezi Disemba

Mgogoro Sahel kuwa sehemu ya ajenda ya Baraza la Usalama UM mwezi Disemba

Rais mpya wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Mohammed Loulichki ametangaza ratiba ya shughuli za baraza hilo kwa mwezi huu ambapo amesema ulinzi na usalama kwenye ukanda wa Sahel barani Afrika ni miongoni mwa mambo yatakayopewa kipaumbele.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini New York, Marekani hii leo baada ya kuchukua wadhifa huo kutokana na India kumaliza kipindi chake cha mwezi mmoja, Bwana Loulichki amesema baraza litaitisha kikao cha ngazi za mawaziri tarehe 10 mwezi huu kujadili changamoto zinazokabili nchi zilizo eneo la Sahel ikiwemo Mali.

Amesema tayari Afrika imetekeleza wajibu kwa kuandaa mpango wa kupatia suluhu migogoro kwenye ukanda huo na kwamba sasa ni wakati wa Umoja wa Mataifa kutekeleza wajibu wake.

Halikadhalika amesema tarehe 12 mwezi huu baraza litakuwa na mkutano wa kupatiwa muhtasari wa shughuli za ulinzi wa amani kwenye maeneo mbali mbali.